Mwandishi: James K. Laurent – Mdau wa Haki za Kidijitali na Usalama wa Kidijitali
Kampeni ya Ulinzi wa Taarifa na Faragha za Watanzania (Data Protection & Privacy campaign in Tanzania) ni kampeni ya mwezi mmoja iliyoanza Julai 2022, inayoendeshwa kwenye vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii ya Twitter na Facebook kupitia kurasa za ‘@ProtectDataTZ’. Kampeni hii inaratibiwa na Bw. James K. Laurent kwa ushirikiano wa karibu na wadau wa haki za kidijitali na haki za kijinsia; Bw. Peter Mmbando – Digital Agenda for Tanzania Initiative (DA4TI), Imani Henrick – Mwandishi wa Habari, Idd Ninga – Dunia Salama Foundation (DUSAFO), Elizabeth James – Mwanasheria, Mihwela Justine – ATPWE na wadau wengine wengi. Kampeni hii ina lengo kuu la kuuelimisha umma wa watanzania kujikinga na changamoto sugu ya utumiwaji mbaya na kuvujishwa kwa taarifa nyeti za watu kinyume na idhini zao. Lengo dogo la kampeni hii ni kuliomba Bunge na Serikali kutunga Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na Faragha za Watu; kwa kiingereza Data Protection & Privacy law. Sheria hii itamlinda kila mmiliki wa ‘data’ ama taarifa nyeti, iwe mtaani au mitandaoni. Wakubwa kwa Wadogo. Wanaume kwa Wanawake. Wenye mamlaka kwa Wasakatonge.
Itakumbukwa, kupitia makala iliyoandikwa na mwandishi Bernard Lugongo wa gazeti la Dailynews mnamo tarehe 7 Novemba 2021, kwenye mkutano wa Jukwaa la Usimamizi wa Intaneti Tanzania (Tanzania Internet Governance Forum), Dkt. Jim Yonazi – Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, alinukuliwa akisema kuwa utungwaji wa sheria ya Ulinzi wa Taarifa, upo kwenye hatua za mwisho.
Kampeni hii imekuja muda mwafaka ambapo tunashuhudia wimbi kubwa la kuvujishwa kwa taarifa nyeti za watanzania pamoja na matumizi mabaya ya taarifa za umma pasi na idhini za walengwa. Baadhi ya mifano ya utumiwaji mbaya wa taarifa za watu ni pamoja na namba za simu za wateja wa mitandao ya simu, vitambulisho vya taifa (NIDA), vitambulisho vya mpiga kura, kadi za ATM, video na picha za udhalilishaji wa kingono almaarufu ‘Connection’, mazungumzo na meseji za siri, vyeti vya matokeo ya elimu ya juu, na kadhalika.
Kero ya jumbe za “Ile pesa tuma kwenye namba hii…”
Bila shaka, kila mmiliki wa namba ya simu Tanzania amewahi kutumiwa jumbe fupi au SMS za kitapeli za: “Ile hela tuma kwenye namba hii…”. Na kama hujawahi, basi mifano mingine ni jumbe za kitapeli kama:
“Jiunge FREEMASON umiliki majumba magali pesa kipaji viwanja ajira masomo ukue kibiashala piga …”.
“Habari za leo mzazi mimi ni mwalimu naomba unipigie haraka sana shuleni kuna tatizo mtoto wako amedondoka ghafla kaumia sana”.
“Mjukuu wangu ndagu niliyokukabizi hiyo uwe makini na pesa hizo zinazokuja usiogope ndio mafanikio yako, si nilikwambia utafanikiwa kwa mda mfupi sasa umeona mwenyewe na siri hiyo usitowe kwa mtu yoyote utajili huo ni mkubwa sana utaweza kuweka miladi ya kira aina popote pale unipigie nikuelekeze.”
Hizo ni baadhi tu ya jumbe za kitapeli ambazo wateja wa mitandao ya simu hupokea kila siku. Kupitia kampeni ya Ulinzi wa Taarifa na Faragha za Watanzania, tunauelimisha umma kuhusu udanganyifu wa hawa matapeli. Hata ukiangalia SMS hizi, utagundua zina makosa mengi ya kiuandishi. Matapeli hawa wamekuwa wakitumia tamaa za watu kutaka kutajirika haraka, ama upendo wa wazazi kwa watoto wao ambao huenda wanasoma shule za bweni, kuwadanganya wazazi wakurupuke kutuma pesa kwa matapeli wanaojifanya ni walimu.
Na sasa hivi matapeli wamekuja kivingine. Wameenda mbali zaidi na kuwapigia simu wateja wa mitandao ya simu wakijifanya wao ni watoa huduma kwa wateja na kuwaomba wateja kurudisha miamala ya pesa zilizotumwa kimakosa, ili mteja atume pesa zake halali kwenda kwenye namba za matapeli. Wengine huwapigia simu wateja na kuwaelekeza kubadili lugha ya huduma za miamala kutoka Kiswahili kwenda Kiingereza ili wawachanganye zaidi wateja na kuwapa maelekezo ya kutuma miamala ya pesa kwao kwa lugha ya kiingereza. Ukweli ni kwamba, wengi wameshatapeliwa na bado wanaendelea kutapeliwa.
Utaratibu wa kusajili namba za simu kwa alama za vidole na namba za vitambulisho vya taifa (NIDA) ulipoanzishwa nchini mwaka 2018, binafsi nilidhani ungekuwa mwarobaini wa utapeli kwa njia ya namba za simu. Hata hivyo, matapeli wameongezeka maradufu. Licha ya jitihada nyingi za Jeshi la Polisi Tanzania kukamata mitandao ya matapeli hawa pamoja na kuwaonya watumiaji wa mitandao ya simu mara kwa mara dhidi ya utapeli wa namna hii kupitia huduma ya kuripoti UTAPELI kwa namba 15040 au kwa kupiga *148*90#, maswali ambayo bado kila mtanzania anaendelea kujiuliza ni, “Hawa matapeli wanapata wapi namba zetu za simu?”, na, “Na kama namba zote za simu huwa zinasajiliwa kwa vitambulisho vya taifa (NIDA) na alama za vidole, kwanini mitandao ya simu haifungii namba za matapeli?”.
Kupitia mijadala ya kila wiki inayofanyika kwenye Twitter Space ya ukurasa wa @ProtectDataTZ, mmoja wa wachangiaji wa mada kuhusu meseji za utapeli alihoji, “Kwanini mitandao ya simu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) wasizuie hizo SMS juu kwa juu kabla hazijamfikia mteja?”.
Tulipopita mitaani pia kuzungumza na wanachi kuhusu maoni yao juu ya hili janga. Janeth Joseph mkazi wa Manispaa ya Moshi alisema,“Hawa watu [matapeli] najiuliza huwa wanapata wapi namba zetu?…Huenda ni watu waliowahi kufanya kazi kwenye kampuni za mitandao ya simu na baadae wanaanza kuvujisha siri za kampuni. Kwahio wanatumia data za wateja na kufanya utapeli wanaoufanya.”
Naye Bw. Ashraf Ramadhani, bodaboda anayeishi pia Manispaa ya Moshi alisema, “Yaani matapeli wao wanachokifanya, wanakisia namba…Meseji ya mwisho ya utapeli niliyopokea ilikuwa inasema; ‘Mwanao anaumwa yuko shule, tuma laki tatu’. Na ukiangalia sina mtoto anayesoma boarding (shule ya bweni).”
Mifano ni mingi sana, lakini mwisho wa siku, suluhu ya kudumu italetwa na Sheria itakayotoa adhabu kali kwa hawa wahalifu na kwa kampuni za mitandao ya simu ambazo hazichukulii kwa uzito wajibu wao wa kulinda namba za wateja wao dhidi ya kero hii ya SMS za utapeli.
Mara ngapi tunaona C.V za watu au makaratasi ya wasifu wa waomba ajira yakiokotwa mitaani na kutumika kama vifungashio? C.V hizo zina tarifa nyeti za waomba ajira. Je, vitabu vya kuandikisha taarifa za wageni mapokezi au kwa walinzi wa ofisi vinatunzwa vizuri?
Na ndio maana Kampeni ya Ulinzi wa Taarifa na Faragha za Watanzania inatoa wito kwa Serikali na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunda rasmi Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na Faragha za Watu (Data Protection and Privacy law). Majirani zetu Kenya na Uganda tayari wana sheria hii.
Ulinzi dhidi ya Udhalilishwaji wa kingono (Connection)
Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na Faragha za Watu pia itawalinda wahanga wa udhalilishaji wa kingono mitandaoni almaarufu ‘Connection’, wengi wao wakiwa wasanii wa kike. Lakini pia kuwapa adhabu kali wanaovujisha maudhui ya udhalilishaji wa kingono mitandaoni na nje ya mitandao.
Wadau wa Kampeni ya Ulinzi wa Taarifa na Faragha kwa pamoja tunakemea na kupinga vikali vitendo vya udhalilishaji wa watu wa hadhi na jinsia zote, iwe mitaani au kwenye mitandao ya kijamii, vinavyofanywa na watu mashuhuri kama Mange Kimambi kupitia mtandao wa kijami wa Instagram pamoja na Aplikesheni yake ya udaku, kuwadhalilisha wanawake wenzake. Tunapongeza hatua ya serikali kuzuia watumiaji wa Tanzania kutumia Aplikesheni hiyo lakini pia tunaipongeza kampuni ya Instagram kuifungia akaunti ya Mange Kimambi tarehe 5 Agosti 2022. Hata hivyo, hatua hizo si za kudumu. Udhalilishaji wa kingono ni doa la kudumu kwenye maisha ya mhanga na athari zake kisaikolojia ni endelevu, kwakuwa maudhui yale hubaki milele mitandaoni, vizazi hadi vizazi.
Kupata dondoo za jinsi ya kujilinda dhidi ya matumizi mabaya ya taarifa zako na farègha, fuatilia Kampeni yetu ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na Faragha za Watu (Data Protection & Privacy Campaign) kwenye kurasa zetu za Twitter na Facebook kwa jina la @ProtectDataTZ .
One Comment
Peter mussa
Utungwaji wa sheria mpya ni muhimu kwa ulinzi wa data,sababu sheria zilizopo zinawanyima watu haki zao za msingi katika utumiaji wa mitandao ‘na ulinzi wa taarifa
Pia elimu kwa jamii kuhusu matumizi ya mitandao ipewe kipaumbele